Kuhusu Kitabu
Makuadi wa soko huria ni hadithi ya kihistoria yenye ukweli unao dhihirika leo iliyoandikwa na Mwandisha Profesa Chachange Seithy L. Chachange. Hadithi hii inatoa taswira ya mapambano ya Watanzania katika kujipatia uhuru na amani ya kweli. Mapamano dhidi ya ukoloni na baadaye dhidi ya baadhi ya watu wao walioteka nyara uhuru wa wengi na kushirikiana na wageni kupora rasilimali ya nchi kwa kisingizio cha soko huria. Hadithi inaweka bayana uozo na udhalimu uliojificha katika mfumo wa soko huria: Tamaa ya pesa na nguvu za kiuchumi; ubinafsi na ukandamizaji. Pia ni hadithi ya matumaini. kuutuonesha Jinsi watu wasivyokubali kukandamizwa, kwamba tamaa. Makuadi wa soko Huria inatukumbusha kwamba utu wa binadamu hauvunjwi kwa pesa wala kwa mabavu.
Mafunzo Kitabuni:
Mtu akiumwa na nyoka, akiona hata nyasi hustuka.
Mapenzi ni mapenzi; hayamfanyi mtu akala!
Hakuna maisha mabaya duniani kama yetu ya upweke kwa mtu mzima na kukosa mguso wa mwili wa mwenzi.
Matatizo ya ubinadamu hayatamshinda Mungu kuyaondoa.
Kumbukumbu ni silaha.
Kujifunza kusahau ni makosa yasiyo sameheka!
Kusamehe ni halali, si kusahau.
Methali moja haina ukweli.
Mwisho wa safari hufikwa baada ya kwenda uendako.
Kumbukeni: ni wale tu walio dhaifu ndio hutamani kuchelewa.
Mwenye busara ni yule mwenye kumbukumbu, akawa nayo moyoni, lakini Mjinga ni yule apayukaye.
Kumbukumbu ni tunu pekee aliyozawadiwa Mwanadamu na viumbe wengine wote wakakosa.
Uzembe hufanya historia ijirudie kwasababu ya kukataa kuya vinjari yale yaliyopita.
Watutsi, Watwa na Wahutu ni watu wamoja.
Mfikila siyo kukubaliana na kila anacho kisema
Mmbumba – mwanamke mtegemezi ambaye ni mhika, yaani mtu baki wa kufikia tu!
Madaba ni jina alilobandikiwa mwanaume aliyeoa au ambaye bado kuoa lakini ana mahusiano ya kudumu ya kimwili ua mwanamke anayeishi nyumbani kwa wazazi wake.
Madaba ni mtu aliyeonekana mara moja moja, na pindi akionekana mwanamke aliyehusika naye alikuwa na uhakika wa kupata pesa za matumizi za kutosha hadi hapo atakaporudi tena.
Watonda, watu wasiojua kuogolea.
Subira huvuta heri, ni tofauti na uvumilivu ambapo mvumilivu huweza kuishia kula mbivu.
Adhabu zikizidi baadaye, huwa majuto.
Kuota ndoto isiyooteka; kupigania maisha ya heshima; na kutumainia na kupigania ulimwengu wenye neema na haki zote za kijamii! Hayo ndivyo yamekuwa matamanio ya Mwanadamu tangu mwanzo wa historia.
Kwakweli, vicheko na tabasamu huficha mengi.
Masikio ndio mlango wa hekima.
Mapenzi kama yapo ni dhana ya kidhaifu.
Utamu wa masimulizi yeyote yale ni tamaa ya kujua baadaye kutatokea nini.
Mbwa mwizi huachia vitoto vyake jina baya.
Kufariki kwa mzee, ni kama kuangua kwa maktaba au hazina ya vito!
Matamanio ya maisha mema ndiyo imekuwa ndoto ya Mwanadamu tangu kutokea kwa ulimwengu.
Ukweli ni kwamba kila mwanamke, anahitaji mwanaume na kila mwanaume anahitaji mwanamke.
Mwenye akili timamu hajifanyi, na mwenye akili timamu huyaoni mambo kama yalivyo na akayakabili kama yalivyo.
Penye wengi haliharibiki neno.
Hakuna matatizo yasiyo na ufumbuzi, wala hakuna mkosaji asiye sameheka.
Kuwa mwanaume duniani ni majaribu makubwa.
Katika dunia hii kuna watu wa aina nyingi, wapo wanaoitaji na wale wanaoyachukia maisha kama yalivyo.
Utamu wa Kiswahili.
“Mimi ni kawauliza rafiki zangu! Lakini mbona hata hiyo Tume imeandika majuzuu na majuzuu? Hayo majuzuu waliyoandika akina Desmond Tutu siyo kumbukumbu itakayo bakia mbele? Kwanini mnipe ushauri kama huo? Je, nani ambaye hajui kwamba kumbukumbu ni silaha? Kama Afrika Kusini wanajifunza kusamehe na kusahau; je haikuwa muhimu kutosahau kujifunza? Nikawakaripia; hata kujifunza kusahau. Nikawakumbusha kutokana na kujaribu kusahau, hata huko Afrika Kusini, madonda yaliyokuwa hayajapona; nayo bado yakitishia kutoa damu tena kutokana na mabaki ya vishina vya miti ya maonevu na uovu; ambavyo bado uliendelea kumea matawi mapya”.
“ Nilitarajia kuanzisha gazeti ambalo lingetoa habari na Makala ambazo zingekuwa kioo cha maisha ya Watanzania, ambalo lingeakisi udhaifu wao na kuwafanya wajikosoe, liwaumbue maaluni, wote wenye uwili wa popo wa kujifanya ndege kumbe ni wanyama, mazandiki na waovu wanaoficha hisia za ubinadamu kwa uhayawani wao. Lisingeishia hapo! Lingerudisha tena nuru ya matamanio ya harakati za maisha ya uadilifu, unyoofu, haki na heshima.”
“Utani ukazuka mitaani kwamba sasa kuna kundi dogo la waandishi wa habari na kubwa la wahandisi wa habari, wahandisi wa habari wasiokuwa na taaluma wala maadili, na kazi yao ni kutunga habari, alimradi ziwe zinauzika katika enzi hizi za kuuzika chochote kinacho uzika.”
“Mtanda Bantu – ama rafiki wa watu kama watu walivyomwita enzi hizo. Huyu alikuwa si mwingine, bali ni yule mwindaji maarufu; Bwana Pieter Pretorius, ambaye shughuli yake kabla ya vita ilikuwa ni uwindaji wa tembo katika bonde la Rufiji na Hifadhi ya wanyama ya selous au shamba la Bibi. Licha ya shamba lake dogo ukingoni mwa Delta, kazi yake kubwa ilikuwa ni uwindaji. Naye alikuwa ameshaua zaidi ya tembo mia sita hadi wakati vita inaanza.”
“ Ama kuishi ni kujifunza! Na hekima ya kujifunza, hususan mahusiano ya watu, ni kuwa mwepesi wa kuhisi.”
”Ndio, vijana wa Kingoni, Kindendeule, Kipungwa na Kibene walikuwa wakiondoka kwa wingi kuelekea Dar es salaam. Alianza Magurumbasi mwaka 1902, akaanzisha makazi kusini mwa bandari ya Dar es salaam, sehemu ambako wengi waliofanya kazi bandarini waliishi ndiyo pale panapoitwa Keko Magurumbasi, Pale penye mbuzi wengi waliozagaa kila mahali, ambao hata wezi huogopa kuwaiba, japokuwa mwenyewe mzee Magurumbasi alishajifia siku nyingi. Ngano zinadai kwamba Magurumbasi aliondoka songea baada ya watu kudai kwamba mama yake ati alikuwa mchawi, lakini hayo hayakuwa na uthibitisho, kwani waliofika Dar es salaam. Kama angekuwa anahusika na mambo hayo ya uchawi, je, angekuwa mkarimu kiasi hicho?
“. . . Haya ndiyo yalikuwa maisha ya kambini, Hakuna kilichokuwa haramu, na la muhimu lilikuwa ni kuhakikisha kwamba mkono unafika kinywani na unaamka asubuhi ifuatayo ukiwa salama. Hapakuwa na ulimbwende wala uchaguzi hapa!”
“Miongoni mwa wanafunzi aliopata kuwa marafiki nao aliwafundisha kwamba tatizo la Tanzania lilikuwa ni kupapukia ujamaa mapema mno, kwani kufuatana na mafunzo ya Mwanafalsafa Karlx Marx, ilibidi Tanzania na nchi zingine ambazo hazijarudisha kusubiri ubepari ujikite juu kutosha, kwa kuwasaidia mabepari wazalendo, ndiyo baada ya hapo ingewezekana ujamaa madhubuti kujengeka.”
“Sasa ningejifunza, haitoshi kabisa kulifahamu jambo. Kuambiwa ni habari tu, unaambiwa na unafahamu, unajua kwamba tukio Fulani limetokea. Gumu zaidi ni kuelewa mantiki ya hilo jambo, na hata baada ya kufikirika na kulifahamu ugumu mwingine huja pale ambapo inabidi ulielezee lieleweke na maelezo yakujitosheleza yenyewe na kumfanya kila asikilizaye kuridhika kwamba jambo linaeleweka na mtu mwengine akauelewa. Hapa Umuhimu wa kufikiria unachukua nafsi za pekee. Hii ndiyo maana ya mawasiliano.”
“Unajua umasikini ni kitu kibaya sana, na ni adui mkubwa wa maendeleo. Hulka ya kimaskini hupelekea watu wakataka wale wote wanaorudishwa nyuma kimaendeleo ili waishi maisha ya kimaskini!”
“. . . Richard Wright, aliyesema kitu kama: Hatari inayoukabili ulimwengu wa leo ni kusahau kile kiainishacho ubinadamu wetu, kitu mithili ya hicho. Alilenga kusema kwamba maana halisi ya mahusiano, maana halisi ya maisha ya binadamu inaelekea kusahaulika. Na hii ndiyo hatari kubwa inayo tukabili leo. Ni mtihani mkubwa: kwani kipimo cha utu si utu tena, bali mienendo na tabia za kikatili na ufisadi. . . . Leo, hii mapenzi ni neno lililobadilika kabisa maana yake, sasa mapenzi ni uhusiano wa mtu na gari au mali yake, mapinduzi limegeuza kumaanisha aina mpya ya sabuni ya kufulia au kuogea iliyoingia mtaani; uhuru na ukombozi yana maanisha uwezo wa kumiliki simu ya mkononi na kadhalika lugha imebadilika kabisa! Neno utu limegeuzwa kuwa kifupisho cha utukufu na ubinadamu ukawa ubwana damu, hata damu imekosa thamani na utakatifu wa asili.”
“Ni wazi kwamba maadui wa binadamu ni wengi kama marafiki zake, na hii ndiyo historia yetu binadamu tangu enzi na enzi. Hivyo, daima tumeishi kwa kutambua kwamba maisha ni pande mbili ambazo daima hukinzana moja ikishinda na nyingine ikishindwa, na baada ya hapo huibuka ukinzani mpya wa aina yake. Lakini katika hayo yote, roho ya maisha yetu haifichwi hata siku moja. Hayo ndiyo yaliyotuleta hapa: Ule umoja wa binadamu, ng’ombe, wanyama wapori na misitu ambayo ni tunu tuliyo kabidhiwa na Mwenyezi Mungu na kuambiwa: “E’nendeni ulimwengu mkaishi kwa busara ya utugemeano!”
“. . . Watu wote wa Pwani na Mrima ni jamii ya Waswahili ndiyo hivyo tuijuavyo historia, kwamba sisi wote ni wamoja na mila na desturi zetu karibia moja tu. Hapo kale tulijua kwamba Waswahili maana yake watu wote wa Pwani na Mrima kwa ujumla kutoka Lamu hadi Mvita, Tanga bandari ya Tanga huta mguu, Lindi, tangu Wadigo na Wasegeju wa Tanga na W’abondei kadhalika watu wa Saadani na jirani za Wadoe na watu wa Bagamaoyo pamoja na jirani za Wazaramo, watu wa Kilwa pamoja na jirani zao Wangindo na watu wa Lindi Pamoja na jirani zao Wayao. Alimradi watu wote kutoka Mogadishu hadi Sofali tulikuwa Wamoja — kimila na desturi.”
“Dunia ingalipo na imekuwepo . . . sisi tunaikuta na tutaiacha; hakuna kitu kama kuchelewa duniani. Ni- wale wenye tu wenye tamaa ndio hupenda. Unadhani kwa nini Mwenyezi Mungu kaivumilia dunia hii mamilioni ya miaka yote hii na madhambi tuliyonayo, kama si busara?”
“ Ushirikiano na ushindani ni vitu vinavyo kinzana na kutengeneza, kimoja hakipo ila ya chenzake. Kadhalika, udhanifu na uyakinifu una uhusiano huo huo!”
“Mwanamke: Alaaniwe aliyeanzisha mapenzi duniani! Kama ningemjua angekuwa adui wangu wa Kwanza!
Mwanaume: Hapana, abarikiwe! huyo ndiye rafiki bora kuliko wote!”
“Kwahiyo tukasema sisi kama wapiga kura ni watu.Tunaotegemeana na wabunge ambao ndio wawakilishi wetu halali. Ukweli ni kwamba, bila raia hakuna watawala, na kinyume chake ni vivyo. Wabunge na raia wanategemeana. Wabunge na watawala kwa ujumla na raia hawatakiwi wawe na uhusiano wa jiwe na nazi,raia na wabunge ni kama mikono miwili ya binadamu.
“kuna mambo muhimu na maalumu ambayo yanalazimu kila mwanadamu wakati fulani ayafanye, mambo ambayo kila mwanadamu mwenye nyama na damu yabidi apate fununu yake. Ububu huzaa mazonge na madhila yanayo zificha roho. Ububu si kitu cha kuambatana nacho kabisa, ni laana asiyoistahili mwanadamu.
“Ibilisi niondokee! Wacha kunitia wasiwasi tena! Ya Rabhi Mola mkwasi apendacho nakuomba, pamoja na mababu, mabibi na mizimu, maisha mema kanijalia, na yaliyopita kuyafutilia mbali! Naomba ya Rabhi nifungue pingu zangu”
“Binadamu ni tofauti na malaika hawaishi kwenye virambo, mitaa, vitongoji, vijiji wala miji, wao hawana mizimu hawana uzao wa kizazi kama sisi binadamu, hawazaliwi wala kufa. Hawana haja kuoa au kuoana na kuzaa watoto, ambao inabidi walishwe. Anga na mbingu zote ni makazi na makao yao. Ziraili na Jibril hawana haja ya kushirikiana. Kila mmoja ana maisha yake na anaweza kuishi peke yake. Binadamu huzaliwa kizazi hadi kizazi, na ni asili yao kutegemeana, kila mmoja akimtegemea mwenzake, na ndipo huweza kulishana, kuleana na kutunzana.”
“Ushindani na ushirikiano si vitu vilivyo kinyume na kupigana hata kidogo. Katika ushindani ndimo ulimo ushirirkiano na katika ushirikiano ndimo ulimo ushindani. Kiondoe kimoja kati ya hivyo kitacho bakia ni mchafuko matupu.”
“. . . Ni uhayawani wa kulana na kutofanana kama wanyama! Na haya ndiyo tuyashuhudiayo sasa hivi.”
“Nenda mjukuu wangu! Neno limetimia, mimi ndiyo niliyekutoa nje mara moja tu baada ya wewe kuzaliwa na kukuonyesha jua. Baba yako alikuwa ametamka maneno pale nje, akasema! Wewe hutaishi uje kuwa manamba au mtumwa kama alivyoishi yeye. Akawaomba mizimu na miungu kuwa ukue mtu mzima, maisha yako yawe ya heri na furaha, kisha wige mfano wa ndege mlembe, uwaongoze watu wema na waadilifu kwenye asali, na mazandiki wote na wale watesao roho za watu kwa nyegere, kile kicheche ambacho hurina asali kwa kumfukuza nyuki kwa ujuzi na kuwafukuza binadamu na wanyama sehemu za ulingo vya siri! Umekuja ulimwenguni lifualo litafute, lieleze na ulieneze! Lisilofaa epukana nalo kabisa! Nilikurudisha ndani kwa mama yako akuonyeshe. Na kwa kuwa hukulia, tukajua kwamba umekubali yale uliyo ambiwa na babu yako. Sasa mjukuu wangu mimi nakwambia. Elimu si Ufunguo wa maisha, bali ukombozi wenyewe. Ukasome kama Nyerere mpaka uwe kama Nyerere!”
“. . . Je, ilikuwa ni halali mambo yafikie hapo yalipofikia, ikawaje, hawa watu dhalili wa Rufiji ambao walikuwa mstari wa mbele katika kupigania uhuru,hawa watu waliokuwa na uzao wa wanawake maarufu na jasisri kama Bibi Titi Mohammedi wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika, wakaishia kuhainiwa baada ya miaka thelathini na mitano ya uhuru? Hadi kufikia mwaka 1955, huyu mwanamke jasiri wa kimatumbi alikuwa amemsaidia Katibu Mkuu wa TANU, Bwana Oscar Kambona, kuwapata takribani wanawake Zaidi ya 5,000 kujiunga na chama akawa ndiyo mhamasishaji mkuu katika kila Mkutano wa hadhara na mzungumzaji wa kwanza kabla Mwenyekiti wa TANU, Bwana Julius Nyerere, hajazungumza na wananchi. Nini kilikuwa kimetokea hadi yawasibu haya?”
Misamiati
Hebedari
Kutoa mbweo – maana yake usije kutengeue udhu hapa kwa kutotolea harufu isiyo pendeza.
Inatosha
Kidhanifu.
Hubedari
Bughudhi.
Ushairi.
Muyaka bin Haji Al-Ghassaniy;
Ulimwengu ukisuka hutoshewa watu pia,
Pasiwe na kukumbuka kuweza jambo la ndia;
Na leo kumechafuka mwaionaje dunia?
Mulioko kongowea, Mwatupa shauri gani?
Tuombeni la kutenda jambo lenye welekeo,
Siku ya kivuno panda waume wakivuvia,
Njeo hizi kutavunda kunukakwe ni viwaga,
Muliozeo kongowea, Mwatupa shauri gani?
Si mwema udanganyifu, atendaye hujutia,
Huitwa mpeketefu, mambo yakinitatia,
Kakumbwa ni uvundifu, kula kukamtukio.
Mulioko kongowea, mwatupa shauri gani?
Wewe Ndiye Nguvu ya Kazi Hii
Kila neno unalosoma hapa limeandikwa kwa moyo mmoja—kwa mapenzi ya hadithi nzuri, maarifa yenye thamani, na maudhui yanayogusa maisha yetu ya kila siku.
Kama umejifunza, kutabasamu, au kujihisi karibu na maneno yangu hata mara moja, naomba upate nafasi ya kuunga mkono kazi hii. Kwa kuchangia kuanzia TSh 1,000 tu, unakuwa sehemu ya safari hii ya kuleta maudhui bora, ya kweli, na yanayojenga.
“Kiasi sio kikubwa, bali moyo unaochangia ndiyo unaojenga.”
Tuma sapoti yako kupitia link hii: https://nisapoti.com/mtandabantu
Na kwa kila mchango—mdogo au mkubwa—najua kuna mtu nyuma yake anayethamini kazi hii. Asante kwa kuwa mmoja wao.
Tunaendelea pamoja.
Mtanda Bantu.