Ruge Mutahaba Ulikuwa Nani?
Uliwaonyesha wengi kuwa tasnia ya burudani si kelele za vijiweni, bali ni jukwaa la fikra, dira ya mabadiliko, na daraja kati ya kizazi na maono.
Kijana mzaliwa katika hospitali ya Alta Bates, California — mtoto wa ndoto aliyechomoza kama mwanga wa alfajiri kutoka familia ya wasomi wa daraja la juu: Profesa Gelase Mutahaba na Dkt. Christina Mutahaba.
Ulikua katika kipindi ambacho jamii iliitazama sanaa, muziki na burudani kama makelele ya wahuni — sekta isiyo na heshima wala mustakabali. Lakini wazazi wako, waliokuwa wakishika mashahada kama vile mikono ishikavyo mishumaa ya maarifa, walichagua kusikiliza sauti ya ndani yako kuliko minong’ono ya mitazamo ya kale.
Wakati jamii waliona muziki kama giza lisilo na mwisho, wao waliona nuru inayoweza kuangaza kizazi kizima. Wakakuruhusu mtoto wao kupanda mlima wa ndoto zako bila kukukatisha miguu, wakaamini maono yako.
Wakati wengine waliona muziki na burudani kama giza lisilo na mwisho, wewe ulikuja ukiwa kama taa ya chemchemi, ukiongoza njia katika uwanja ambao haukuwa na ramani. Hukuwa muimbaji, bali ulikuwa mchoraji wa ramani — Jasiri uliyechonga njia kwenye mwamba wa dharau za kijamii, ukiamini kuwa sanaa ni sauti ya taifa.
Uliwaonyesha wengi kuwa tasnia ya burudani si kelele za vijiweni, bali ni jukwaa la fikra, dira ya mabadiliko, na daraja kati ya kizazi na maono. Wewe hukuwa sehemu ya muziki kwa kutengeneza pesa, bali kwa maono; hakupiga ala za muziki, bali uliwasha taa za jukwaa kwa wengine wang’ae.
Kama ilivyo desturi, ni furaha ilioje kwa mama baada ya miezi tisa; ya uchungu, adha, mateso na wengine hata kuvimba sura na kubadilika maumbile yao ila vyote hivyo usahaulika na kusherekea kuona kile kiumbe kilichofamfanya aipitye hayo. Hata kwa mama Christina Mutahaba ilikuwa hivyo pia.
“Nilipojifungua Ruge, nilifurahia sana, kurukaruka, kama wazazi wengine wanavyokuwa, unategemea atatusaidia ; atatuendeleza, kumbe kwa kudura za mwenyezi Mungu. Akampa uwezo wa kuwasadia hata wengine ambao walikuwa si kwenye familia yetu.”
Ruge Mutahaba ulizaliwa kutupatia vitu vitatu: Uliandika historia; kutuachia kumbukumbu; na uIlitutendea wema uliotukuka. Na katika wema uliotukuka ulizidi kutuhasa tusiwe watu wa kupenda ndoto ndogo; maana zitafanya tubweteke ila tukiwaza mambo makubwa yatatunyimayo usingizi na kufanya tushughulikie ndoto zetu na hatimaye jamii itabadilika kupitia sisi na katika moja ya sehemu ya mazungumzo yako na vijana pale Chuo kikuu cha Dodoma mwaka 2017 ulitusisitiza pia kuwa: “I dont like small thinking, I don't like small dreams; I like big dreams, and you will never be able to achieve your dreams– nakuambia ikiwa ndogo, never! Na bora usiipate. Lakini pigana – wanasema pigana kuwa jua kwa sababu hata ukishindwa utakuwa nyota… ”
Kama tunavyofahamu safari yako Ruge Mutahaba, ilianza na urafiki wako na Joseph Kusanga; safari ya iliyokuwa na mabonde mengi; kutokuaminika lakini ilibidi lengo lenu litimie, ili tanzania inufaike leo. Na rafiki yako na mbia wako kibiashara bwana Kusaga anakuelezea vyema; japo alishawahi kukutania kuwa wewe ni mtoto wa kishua; hujui hata kupika ugali ila mpaka sasa hatuna hakika na hilo. Ila kuhusu weledi, uchapakazi na maono huenda tukatanabaisha na haya ndiyo anavyokuzungumzia: “Nafikiri leo nimepata nafasi ya kuweza kuzungumza mawili matatu yanayomhusu — mimi naweza kumuita alikuwa mdogo wangu, rafiki yangu, alikuwa patner wangu Ruge Mutahaba. Nilikutana na Ruge miaka 25… 26 iliyopita nyuma. Wakati huo Clouds ilikuwa inapiga madisko sana — yani tulikuwa tumejikita sana sana kwenye madisko na studio; wakati ule ‘Mawingu Studio’ na madisko. Lakini kutokana na interest, na yeye wakati ule anasoma; kwahiyo kila akija — akija Tanzania anakuja na muziki na wakati ule mziki, unajua kilikuwa kitu adimu sana ni kama mtu analeta dhahabu kwa sababu ilikuwa hakuna access ya kununua wala — kama sasa hivi mna spotify sijui mna nini! Enzi hizo kulikuwa hakuna vitu kama hivyo lakini ni watu ambao tuli-hustle sana kulia, kushoto kwa vita vingi ambavyo tulipigwa. Lakini ki-ukweli tuliweza kusimama imara, alishiriki kwa kiasi kikubwa sana kujenga misingi imara ambayo leo ameacha watu wengi wanaendelea mpaka leo; kuhakikisha gurudumu linasonga mbele.”
Labda naweza kum-describe kwa vitu vitatu; vinne; vitano — lakini acha nizungumze vitu vitatu kwanza: Jasiri; mthubutu; na mtekelezaji”
Kutokana na uhodari wako, wakuona msitu badala ya mti; mbali ya macho yako kuliko vidole vya miguu yako ulijijengea marafiki wengi wa kalba kama yako . Na haiba yako ya kufikika na watu wengi walisema kipindi cha maombolezo yako hata kama ni namba ngeni huwa unajibu ujumbe mfupi hata kupokea simu ngeni na Mheshimiwa Hamisi Kingwangala ni shahidi wa hilo.
Ila rafiki yako Nape Mosses Nnauye yeye anakuamini katika falsafa ya mtu kwenye kujitafutia suluhu ya matatizo na changamoto — maana suluhu ya kweli haipatikani nje bali ndani ya mtu mwenyewe. Na yeye alisema haya kuhusu hilo la kijipatia suluhu: “Ruge aliamini kwamba kila mtu kwenye mazingira yake kuna majibu ya matatizo ambayo anayokabiliana nayo! Hakuamini kwenye mtu mwengine kukuletea majibu, ndiyo maana kwenye programu maarufu sana ile ya ‘Tunakufungulia Dunia, Kuwa Unachotaka,’ Ruge alikuwa muumini kabisa; kwamba kuna kazi ya kukufungulia tu dunia lakini kuwa unavyotaka wewe – ni wewe unaamua uende wapi.”
Kweye hilo la kutafuta suluhu ya changamoto zetu; ukahakikisha ile kasumba katika taasisi; shirika za serikali na binafsi – ya kutoamini vijana, kwako ikakosa nafasi; ukawaamini; ukawapa nafasi – baadhi yao walichekwa, lakini wewe uliwapa mbinu, kuwatia moyo; ulikuwa sikio lao na mfariji wao na kuwaambia wazidi kupambana ili leo yao iwe bora kuliko jana; na kesho yao itakuwa bora zaidi.
Vijana ni wengi waliowapa nafasi, kina Aman Martin, kijana hodari sana, ambaye pia alitumika katika kuandika hata makala ya kutoa taarifa ya kifo chako katika mitandao ya kijamii aliandika yeye — ila kwa ujuzi na silaha ulizompa leo ni mtaasisi katika kitengo cha digitali benki ya NMB; tukiachana na huyo kuna mtangazaji Cza; kijana mdogo uliyemchukua tangu akiwa kidato cha tano; uliyemlea na kumkuza vyema, na hatimaye akaweka rekodi ya kijana mwenye umri mdogo zaidi kushika nafasi ya Mkurugenzi wa Ubunifu katika chombo kikubwa cha habari nchini na ulichokiazisha CMG ( Clouds Media Group); Cza anaamini kuwa ulikuwa kiongozi; na si kiongozi tu, bali kiongozi bora usiye hitaji cheo ili uweze kuongoza.
Cza anakuelezea kuwa wewe, “ Ni kiongozi ambaye kwanza aliamini kabisa kwamba mafanikio namba moja ya kiongozi ye yote yule ni kutoa nafasi kwa wale anao waongoza; kuwa tambua uwezo wao na kukua. Na si ajabu ni kwa namna gani hata baada ya miaka kadhaa ya kuondoka kwake bado ameendelea kukumbukwa na kuwa celebrate na vijana wengi sana ambao wapo kwenye tasnia tofauti tofauti; kuanzia muziki, burudani, media, ujasiriamali na maeneo mengine mengine.
Sasa ilibidi uipende Tanzania na watu wake kuliko chochote kile, ukaanzisha kampeni nyingi zinamhusu Mtanzania wa kila ngazi. Hukubagua dini, kabila wala itikadi za vyama vya kisiasa. Hii inanionesha pale nilipouona usuhuba wako wa dhati wa Nape na Makamba ambao ni wana-CCM; ukaomba upatanishwe na mmalize tofauti zenu, wewe na Bw. Joseph Mbilinyi (Sugu) aliyekuwa Mbunge wa Mbeya mjini kwa tiketi ya chama cha CHADEMA– ukamfata Mhe. Tundu Lissu. Ila hukuacha nyuma ACT Wazalendo. Na hivi mwazilishi wa chama cha ACT Wazalendo, Bw. Zitto Zuberi Kabwe anavyokuelezea ulivyoweza saidia kufanikisha kampeni ya Leka Dutigite.
“Nilikuwa nimejadiliana na baadhi ya wasanii wa mkoa wa Kigoma — wanaotoka mkoa Kigoma; kwa ajili ya kutunga wimbo ili kuweza ku-promote mkoa wa Kigoma. Wimbo ambao baadaye ulikuwa maarufu sana — ukiitwa Leka Dutigite. Kwa hiyo niliamua kuzungumza na Ruge aweze kutusaidia kwa ajili ya kutumia studio za THT kwa ajili ya kurekodi wimbo ule. Wimbo ule niliutunga mimi, pamoja na maeneo mengine wasanii waliohusika. Baada ya wimbo ule ku-hit sana, tuliona kwamba kuna haja ya kuendeleza kundi lile la Leka Dutigite kwa ajili ya shughuli nyengine za kuweza kuwa nufaisha wasanii wenyewe. Tunasherekea maisha ya Ruge kwa sababu aliyaishi maisha ambayo yameacha alama na kwa sisi ambao tulikuwa rafiki zake ni wajibu wetu kuweza kuhakikisha kwamba wakati tuko hai tunaendeleza yale ambayo alikuwa anayafanya.”
Hukushika chaki lakini ulikuwa mwalimu, hukuwa na ngazi lakini ulitupandisha juu. Hekima na busara zako zikafanya wengi walio mashuhuri kuweza kufika pale kwa elimu yako isiyo kuwa na uchoyo wala ubaguzi. Na huyu ni mmoja wa wanafunzi wako Doris Mollel aliyekuwa mlimbwende wa Tanzania mwaka 2012 kwa taji la Miss Universe, “Nakumbuka nilikutana na Ruge ilikuwa mwaka 2015 mwishoni; na nilikutana naye kupitia Hadson Kamoga ambaye alikuwa hapa kama mmoja wa watangazaji wa 360 (Kipindi cha 360); na Hadson Kamoga nilikutanaye wakati nilipokuwa shule wakati nasoma Chuo cha Diplomasia.
Kwahiyo nikamueleza nia yangu kwamba natamani sana kukutana na Ruge; kwamba naamini nikikutana naye ataweza kusaidia agenda ya ‘Mtoto Njiti’ ipate nafasi. Na Hadson hakuwa na tabu ya kuniunganisha naye; akaniambia ‘Doris tayari nishaongea naye, jitahidi uende kumuona ofisini.’ kwahiyo akanipa mpaka muda, nikaenda kumuona Ruge. nakumbuka kitu cha kwanza alichoniambia — aliniambia: ‘Nimekuona kwenye Miss Tanzania na unafanya kazi nzuri lakini you need a support; unahitaji kuwekwa kwenye platform, ujulikane na kazi yako ieleweke. Kwahiyo baada ya hapo historia ikabadilika akaniambia Doris sasa niandikie barua; proposal leta clouds nitaipitisha na tutakusaidia.
Na kitu kimoja kuhusu Ruge, mimi naweza kusema Ruge ni mwalimu; yani mimi Ruge amekuwa mwalimu wangu; kwenye ualimu huo alitanguliza utu. Kwahiyo hiko ni kitu nitaondoka nacho, na nitatembea nacho.”
Hukuwa ndugu yetu wa kuzaliwa lakini ulitupenda; hukuwa mjenzi lakini uliweza kutuchongea barabara ambayo haikuchagua waliopata elimu kwa ngazi ya msingi, sekondari, stashada, shahada, Shahada ya Uzamivu na uprofesa hata wale ambao hawakupata neema ya kupata elimu kabisa, na huyu hapa Mhadhiri anakuelezea vyema, “Naitwa Suma Mwaitenda, niko pale chuo kikuu Ardhi, nafundisha kama Mhadhiri Msaidizi Idara ya Uhandisi. Nipo pale takribani miaka zaidi ya kumi sasa lakini kwa kipindi kile nilikuwa mratibu wa jukwa la Fursa; au platform ya Fursa ambayo ni jukwaa la ujasiriamali kwa vijana — lilikuwa lengo kubwa kabisa la kufungua fursa kwa vijana wa kitanzania.
Binafsi Ruge aliamini kwenye uwezo wangu; Ruge alikuwa anampa kila Mtu – kila nafasi ya kuweza kuonesha nini unaweza kufanya.
Kwahiyo hili ni suala zuri sana katika kukujenga. Kuna vitu vingi ambavyo nafanya sasa hivi — au nimeingia, sijui angekuwepo angeweza kuniambia nini! Lakini naamini angeweza kunitia moyo na kuniambia ‘ Sky is not a limit’, kwamba unaweza fanya; au fanya kwa namna hii bora zaidi. Ko, naweza kusema hicho ni kitu ambacho nina kosa.
Na nilijifunza namna tofauti ya kufanya kazi kwa maana kwamba kama kuna wazo mnakaa wote mnalijadili mezani; mnachambua; kila mtu mchango wake ulikuwa una umuhimu.”
Ujasiri wako ulikuwa wa kipekee na ulikamata tochi kila kwenye giza ili wengine tuone njia. Na ndiyo maana kwa pamoja tuliamini ni jasiri muongoza njia. Na huyu hapa ni mmoja ya mwanao kipenzi ulikuwa unakula naye, na kunywa naye, mwenye kwenye kwa ushuhuda wake katika kipindi cha Salama Na aliishuhudia ulimwengu; kuwa ulimuonesha mapenzi kama mtoto wako wa kumzaa na moja ya hekima uliompatia ni ile ‘usicheke na mtu anayekutukania mama yako’ hii nayo ni hadithi ya siku nyengine ila na kupitisha huku kote ili uje kujibu swali langu, hivi mwalimu wangu ulikuwa ni nani? Basi mwanao kipenzi Barnaba kutoka kuokota siso leo hii yupo hapa kwenye kilele cha mafanikio na anakuzungumzia vyema kwa malezi, hekima na upendo wako uliompatia kwenye maisha yake binafsi na sanaa yake.
“Mimi ukiniambia nikuambie tafsri ambavyo alikuwa mentor kwenye tasnia ya burudani na muziki kwa ujumla; na namna gani amebadilisha maisha ya wasanii katika namna moja kwenda nyengine; au talent na vipaji vya vijana wengi kwenye taifa hili au kwenye nchi hii; kutoka kuwa kivutio cha kawaida na kuwa biashara na kuwa ukombozi katika maisha yao na kujitengeneza ajira ni kiasi kikubwa na hata nisizunguke kwenda mbali mimi ni mfano ulio hai.
Hakuwa tu boss, he was my dady — alikuwa zaidi ya baba yangu mlezi ambaye amenilea; ameni-support; amenikuza. Amenifundisha muziki; amenifundisha maisha ya mziki; na discipline ya muziki; amenifundisha kujiandaa kisaikolojia kwenye kuishi kwenye muziki; na amenifundisha biashara ya muziki na maisha ya muziki natakiwa kuishi vipi, namna gani naweza ku-participate kwenye jamii yangu ya muziki”
Marefu yako mengi ambayo tuliyategemea kwa miaka mingi hatimaye yalipata ncha; muda ulifika; ukatuaga; na ukaondoka. Ulikuwa mkulima mzuri mbegu ulizozipanda zinamea vyema hivi sasa.
Ila Ruge japo ni miaka sita imepita bado nimejawa na raghba ya kutaka kujua wewe ulikuwa nani, Mwalimu? Na je! Ulikuwa na saa ishirini na nne, kama mimi? mbona umeishi maisha mengi na kugusa watu wengi kuliko umri wako?
Je, ulikuwa kiongozi wa siri wa kiserikali? mana sote tulishuhudia, Rais, Makamo wa Rais, hata Waziri Mkuu, walikuja kuhani na kuomboleza msiba wako; naibu spika; mawaziri, wabunge; viongozi wa taasisi na mashirika walihudhuria na hata mama yako alisema alifajirika na kujiuliza uliwatendea nini watanzania? Mpaka waka kupenda vile?
Ulimwengu ulishangazwa na taarifa ya kifo chako, majira ya saa mbili usiku, Hayati Magufuli alipo habarisha ulimwengu juu ya kifo chako, akiwa ni mtu wa kwanza, kutoa habari iliyo tujeruhi fuadi zetu; habari ilifanya tukose maneno ya kutosha kuelezea maumivu na huzuni tuliokuwa nayo, Nchi ikasimama, Tanzania ikazizima kumpoteza mwana mwema wa taifa hili. Na hizi ni baadhi za ujumbe kutoka kwa Rais kwa wakati huo na watu mashuhuri nchini na nje ya mipaka yetu ya Tanzania: “Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha kijana wangu Ruge Mutahaba. Daima nitamkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika tasnia ya habari, burudani, na juhudi za kujenga fikra za maendeleo kwa vijana. Poleni wanafamilia,ndugu,jamaa na marafiki. Mungu amweke mahali pema, Amina.” Magufuli alichapisha ujumbe huu kwenye mtandao wake wa X kwa kipindi hiko ukiitwa Twitter.
“Kwa sasa, dua na fikra zangu ziko kwa Mama, Dkt. Mutahaba, ndugu, na marafiki waliopambana sana kuhakikisha anapona. Nikipata nguvu, nitasema zaidi. Tangulia, jamaa yangu, tunakuja. #RIPRuge” – January Makamba
Rais mstaafu Jakaya kikwete akaelemewa umemtoka rafiki yako unafikri angesema vipi? Wakati alikuacha ukiwa katika hali ya kuridhisha, mara ya mwisho alipo kukutembelea hospitali nchini Afrika ya Kusini… bibi yangu ana msemo wake hakuna ayajuaje baada ya sekunde moja nini kitajiri.
“Nimelemewa! Nakosa maneno ya kuelezea huzuni na majonzi niliyonayo kwa kifo cha Ruge Mutahaba. Taifa limepoteza kijana wake mahiri, mbunifu na mzalendo wa kweli. Nimepoteza rafiki, mshirika mwaminifu na mtu ambaye amenisaidia kwa mengi ktik uongozi wangu na hata baada ya kustaafu.” Mzee Jakaya alishindwa kustahimili, alikiri kuumizwa — Ulikuwa nani Rugemalila Gelase Mutahaba?
Maono yako Ruge; ushawishi wako bado na baki njia panda, nakubaki na swali hili ulikuwa nani mwezetu? Uliona nini ile siku 2010, ambayo licha ulikuwa upo safirni uliweza kumuandikia barua pepe rafiki yako kipenzi January Makamba kuwa ni kwanini achukue fomu ya kukogombea Urais kwa kupitia chama chake cha CCM, mwaka 2015: January Makamba anasema, “Mtu wa kwanza kuweka kichwani mwangu wazo la kuchukua fomu kubwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 alikuwa Ruge Mutahaba. Alifanya hivyo mwaka 2010, miaka mitano kabla, katika email hii aliyoniandikia akiwa safarini Marekani. Na alitoa sababu zake nzito.” Huenda hili swali naweza kukuuliza siku nyingine? Ila hili naomba ulijibu, Ulikuwa nani?
Au niamini kwa jinsi alivyokueleza rafiki yako inanipa picha ya kwanini uliweza kuwa naye kama rafiki yako na msiri wako, na kwake ukajitoa na kuwa dhaifu wa kihisia kumuuleza hofu, mashaka na wasiwasi wako..
“Ukitaka kumkumbuka Ruge siku ya leo; au wakati wowote huendi kwenye kaburi lake kule Bakoba bali unaenda kwenye mafanikio, hisia na alama aliyoiacha kwa vijana wengi katika nchi hii — kwenye tasnia zote: Sanaa; biashara; ubunifu na kadhalika. Vijana wengi wamefanikiwa kutokana ushauri wake; msukumo wake; hamasa yake; na mfano wake vilevile. Na mimi ni mnufaika wa hamasa, msukumo, ushauri wa rafiki yangu Ruge! Tumekuwa marafiki wa karibu sana; tumeongea vitu vingi; tumefanya vitu vingi pamoja; tumeshauriana mambo mengi na kweli sitakuja kumsahau hata kidogo.”
Sebastian Maganga ana lipi la kusema zaidi kumuachia msemo ambao tunatumia katika kizazi hiki na kizazi kijacho ya kuwa ‘Tuogope Mungu na teknolojia.”
“Tulikutana kwa mara ya kwanza mwaka 1997 na kutoka huko tulikutana mara kadha wa kadha katika maeneo mbalimbali. Hapo nilikuwa bado sijawa sehemu ya Clouds kwa maana ya Mcloudsania. Kwanza alisema jambo la kwanza kabisa na sitakuja nisahau kwamba kadiri unavyotengeneza rekodi mpya; wewe mwenyewe una jukumu la kuvunja rekodi yako. Kwahiyo, rekodi yako ya leo haiwezi kuwa rekodi ya kesho; ukishaivunja rekodi yako ya leo uanze kufanya kazi kuhakikisha kwamba rekodi yako ya kesho inavunjwa vilevile. Ukianza kumzungumzia Ruge Mutahaba leo; labda utahitaji miaka mia mbili ya kumaliza sifa zake. Kuwa mwepesi wa kumuogopa Mungu na kuwa jirani kuiogopa teknolojia.”
Sasa nadhani kupitia baadhi ya machapisho niliyo soma kupitia mtandao wa X, kwa watu maarufu na mashuhuri, sasa wamejibu swali langu. Wewe ni mwana mkubwa wa Taifa. Ulikuwa mtu wa kipekee, mwenye fikra pana, mdadisi, na msikivu zaidi kuliko mzungumzaji. Daima ulitafuta mawazo mapya na suluhisho. Ulimiliki sanaa na sayansi ya kufanya mambo yatokee. Na kwa hakika nimeamini thamani ya miaka yetu ni matendo tuyafanyao na si maisha mengi; umeondoka kama mtaasisi mwana wa mageuzi. Ukishughulika na watu vyema na kwa heshima, watakurudishia mara dufu. Hii ni kanuni ya maisha isiyoweza kukosea.
Maana wamefariki watu mashuhuri na maarufu wangapi nchini? Lakini ukimtoa Mwalimu Julius Nyerere, na Hayati Magufuli hakuna mwingine ambaye Watanzania tumemlilia kwa huzuni kubwa na kumpa heshima ya dhati kama tulivyo kulilia wewe Ruge Mutahaba.
Na ningekuwa karibu na Profesa Mutahaba ningemfariji hivi mzee wako: Futa machozi, baba, kisha pokea shukrani za Tanzania. Ahsante kwa kutuletea Ruge, ahsante kwa uzao wako. Tutasherehekea maisha ya mtoto wako, tukikushukuru wewe, Profesa Mutahaba, kwa malezi yaliyomfanya kuwa jasiri, muongoza njia.
Baada ya kushuhudia mapokezi yako Dar es salaam na Bukoba, Kagera; vijana kufagia barabara, wa mama kukutandikia khanga, kutengeneza mabango; Mtu ambaye hukuwa na wadhifa wowote serikalini, wala ambaye sio mgombea Urais. ninatamani kwa dhati ya moyo wangu, sasa kuliko wakati mwingine wowote, nimechagua heshima kuliko pesa na umaarufu.
Safari ya maisha yako, na ulivyogusa wa watu kweli nimeamua kuchagua kuheshimika na kuishi kwenye mioyo ya watu. Mtu wa nyuma ya pazia mwenye hitimisho la kishujaa kama mwangaza wa jukwaa.
Ahsante, Mwalimu wangu, sasa nimejua ulikuwa nani.